Licha ya takwimu na mienendo ya sasa, ripoti ya mwaka huu pia inachunguza dhana ya mazingira ya magereza ya urekebishaji na inasisitiza juhudi za Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuitekeleza kwa vitendo.
Haya hapa ni mambo matano muhimu kutoka katika ripoti hiyo:
1. Idadi ya wafungwa duniani inaendelea kuongezeka
Baada ya kupungua kwa muda mfupi wakati wa janga la coronavirus“>COVID-19, idadi ya watu walioko gerezani imeongezeka tena, na kufikia watu milioni 11.7 mwaka 2023.
2. Magereza mengi duniani yana msongamano mkubwa
Zaidi ya asilimia 60 ya nchi 181 zilizotoa takwimu zinaendesha magereza yaliyofikia au kupita uwezo wake wa kuchukua wafungwa (100%).
Zaidi ya nchi 1 kati ya 4 zinafanya kazi kwa zaidi ya asilimia 150 ya uwezo wa magereza yao.
Msongamano sio tu tatizo la nafasi finyu, bali pia huathiri lishe, usafi, huduma za afya, usambazaji wa magonjwa ya kuambukiza, huduma kwa makundi hatarishi, afya ya mwili na akili, na upatikanaji wa shughuli za maendeleo.
Kupunguza msongamano ni hatua ya kwanza muhimu ili kuwezesha magereza kutekeleza jukumu la kurekebisha wafungwa.
3. Takriban theluthi moja ya wafungwa duniani wako rumande (hawajahukumiwa)
Zaidi ya watu milioni 3.7 wako rumande duniani – sawa na asilimia 30 ya wafungwa wote.
Kanda zilizo na viwango vya juu vya wafungwa wasiohukumiwa ni Afrika na Oceania (asilimia 37), huku Ulaya ikiwa na kiwango cha chini (asilimia 19).
Asia ya Kusini ina hali ya kutia wasiwasi, ambapo asilimia 64 ya wafungwa wako rumande – ongezeko kutoka asilimia 54 mwaka 2013.
Rumande inapaswa kutumika pale tu ambapo kuna ushahidi kamili wa mtuhumiwa kutoroka, kufanya kosa jingine au kuingilia mwenendo wa haki. Kutumia rumande kupita kiasi kunachangia msongamano wa magereza na kuhatarisha haki ya mtuhumiwa ya kupata kesi ya haki.
4. Vifo gerezani vingi vinaweza kuzuilika – zaidi ya kisa1 kati ya 10 ni kujiua
Kwa nchi nyingi zenye taarifa, kiwango cha mauaji ya makusudi kiko juu kwa wafungwa kuliko kwa watu wengine.
Marekani, kiwango cha vifo kwa mauaji kwa kila wafungwa 100,000 kilikuwa 17.4, ikilinganishwa na 2.0 barani Ulaya.
Vifo vya kujiua vilifikia 32.9 kwa kila wafungwa 100,000 mwaka 2023 – zaidi ya mara tatu ya kiwango cha vifo vya kujiua kwa watu wote (9.1 kwa 100,000 mwaka 2021).
Hii inaonesha changamoto kubwa kwa nchi katika kutimiza wajibu wao wa msingi wa kuhakikisha afya na usalama wa wafungwa.
5. Urekebishaji wa wafungwa unahitaji mazingira muafaka
Urekebishaji na ujumuishaji wa wafungwa katika jamii ni sehemu muhimu ya usimamizi wa magereza.
Ushahidi unaonesha kuwa mafanikio haya hutegemea sio tu programu, bali pia mazingira ya heshima, utu na msaada wa mabadiliko ya kweli.
Hii inahusisha:
- muundo makini wa magereza,
- usimamizi ulioratibiwa,
- wafanyakazi walio na malengo ya pamoja,
- sera zinazounga mkono ajira baada ya kifungo,
- na kupambana na unyanyapaa wa kifungo.
2025: Mwaka wa hatua za mageuzi ya magereza na adhabu
Ripoti hii imetolewa tarehe leo 18 Julai – Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela – ikiwa pia ni maadhimisho ya miaka 10 ya Kanuni za Nelson Mandela na miaka 15 ya Kanuni za Bangkok kwa ajili ya wanawake gerezani.
Mwaka huu wa kumbukizi maradufu haupaswi kuwa tu wa kusherehekea, bali unawapa wanajamii wa kimataifa fursa ya kujitolea upya kwa mageuzi ya mifumo ya adhabu na magereza – kwa manufaa ya wote.
Ingawa changamoto zinazozikabili magereza duniani ni kubwa, kuna msukumo unaoongezeka wa kufanya mageuzi. UNODC tayari inashirikiana na zaidi ya Nchi Wanachama 50 katika juhudi za kugeuza magereza kutoka kuwa maeneo ya adhabu na kutengwa hadi kuwa vituo vya haki na urekebishaji.
Hii ni fursa ya dunia kuonesha upya dhamira ya kufanya mageuzi kwa manufaa ya wote. UNODC tayari inashirikiana na zaidi ya nchi 50 kugeuza magereza kutoka sehemu za adhabu kuwa maeneo ya haki na urekebishaji.