Katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa hotuba maalum akisisitiza umuhimu wa kuendeleza maadili na maono ya Mandela ya amani, haki na utu wa binadamu.
“Maisha ya Madiba yalikuwa ushindi wa hali ya juu wa roho ya kibinadamu,” amesema Katibu Mkuu. “Alivumilia dhuluma na ukandamizaji wa hali ya juu, lakini hakujibu kwa kisasi bali kwa maridhiano, amani, na mshikamano.”
Katibu Mkuu amekumbusha kuwa urithi wa Mandela sasa ni jukumu la kila mkazi wa dunia. Amesema kuwa moja ya mafundisho makuu kutoka kwa maisha ya Mandela ni kwamba mamlaka si mali ya mtu binafsi bali ni chombo cha kuwainua wengine.
“Madaraka ni kuhusu watu — na kile tunachoweza kufanikisha pamoja, kwa ajili ya kila mmoja wetu,” ameongeza.